News

ULEGA AWAELEKEZA MAMENEJA WA TANROADS KUTEKELEZA MIRADI YA BARABARA

ULEGA AWAELEKEZA MAMENEJA WA TANROADS KUTEKELEZA MIRADI YA BARABARA

Dodoma, 03 Juni, 2026

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewaelekeza Mameneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) katika mikoa ya Kagera na Pwani kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika utekelezaji na usimamizi wa miradi ya barabara ili ikamilike kwa wakati na kuendelea kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Akijibu swali bungeni leo lililoulizwa na Mbunge wa Misenyi, Laurenti Kyombo, aliyetaka kujua ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Katoma–Bukwali kwa kiwango cha lami, Waziri Ulega amesema Wizara kupitia TANROADS inaendelea na utekelezaji wa mradi huo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Amesema kuwa kati ya kilometa 39 za barabara hiyo, kilometa 8.2 tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami, huku kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu iliyobaki zikiendelea.

“Namuelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera kuhakikisha anaweka kipaumbele katika utekelezaji wa barabara ya Katoma–Bukwali ili kuharakisha maendeleo ya wananchi na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi,” amesema Ulega.

Aidha, Waziri Ulega amesema barabara ya Makofia–Mlandizi–Mzenga ni muhimu na ya kimkakati kwa kuwa ni njia mbadala ya Barabara Kuu ya Morogoro, inayorahisisha usafiri na usafirishaji kati ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Kutokana na umuhimu huo, amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani kuhakikisha anamsimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza ukarabati wa barabara hiyo, ambayo imeathiriwa na mvua, ili irejee katika hali nzuri na iweze kupitika katika misimu yote ya mwaka.

Waziri Ulega amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara nchini kwa lengo la kuimarisha usafiri na usafirishaji, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji, pamoja na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.