BARABARA NI KICHOCHEO MUHIMU CHA UTEKELEZAJI WA DIRA YA MAENDELEO 2050- AISHA
Mwanza, 03 Juni, 2026
Kaimu Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Aisha Malima, ameshiriki katika kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) kinachoendelea jijini Mwanza, ambapo alishiriki katika majadiliano kuhusu namna ya kuwasiliana kwa umma kuhusu miradi ya miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege vinavyosimamiwa na TANROADS.
Majadiliano hayo yaliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mhe. Gerson Msigwa pamoja na viongozi wa TAGCO na wataalamu wa mawasiliano kutoka taasisi mbalimbali za umma nchini.
Akichangia mada hiyo, Malima alisema kuwa mawasiliano ya umma yana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya miundombinu na manufaa yake kwa maendeleo ya taifa.
Alieleza kuwa TANROADS imeendelea kutumia mbinu mbalimbali za mawasiliano ikiwemo vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, tovuti, mikutano ya wadau na kampeni za uelimishaji ili kuwafikia wananchi na kuongeza uelewa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
“Ni muhimu wananchi wakaelewa kuwa barabara si njia za usafiri pekee, bali ni miundombinu inayochochea biashara, uwekezaji, utoaji wa huduma za kijamii na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Hivyo, mawasiliano yetu yanapaswa kuonyesha matokeo chanya yanayotokana na uwekezaji huo,” alisema Malima.
Aliongeza kuwa barabara bora huwezesha wananchi kufikia masoko kwa urahisi, hupunguza gharama za usafirishaji, huimarisha huduma za afya na elimu, na kufungua fursa mpya za uwekezaji na ajira katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika mjadala huo, Malima alisisitiza kuwa sekta ya miundombinu ni moja ya nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwani inatoa msingi wa ukuaji wa uchumi wenye ushindani na maendeleo jumuishi.
“Tunapoelekea Dira 2050, ni muhimu kuendelea kuwasilisha kwa wananchi mchango wa miundombinu katika maendeleo ya taifa. Barabara zinaunganisha watu, bidhaa, huduma na fursa za kiuchumi; hivyo ni kichocheo katika Dira 2050.