News

UJENZI WA BARABARA YA NORANGA–ITIGI WAFIKIA ASILIMIA 83, WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WAKE

UJENZI WA BARABARA YA NORANGA–ITIGI WAFIKIA ASILIMIA 83, WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WAKE

Singida, 02 Juni, 2026

Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Japherson Nnko, amesema ujenzi wa barabara ya Noranga–Itigi yenye urefu wa kilometa 25 kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 83, huku kilometa 20 zikiwa tayari zimekamilika na kilometa tano zilizobaki zikiwa katika hatua za mwisho za uwekaji wa tabaka la lami.

Mhandisi Nnko ametoa taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliyefanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo.

Amesema mradi huo unaanzia Noranga katika eneo la Doroto hadi Itigi eneo la Mlongojili kwa urefu wa kilometa 25 na ni sehemu ya barabara kuu inayounganisha Mbeya, Chunya, Makongorosi, Rungwa, Itigi na Mkiwa yenye jumla ya takribani kilometa 524.

Mhandisi Nnko ameeleza kuwa sehemu ya barabara kutoka Mbeya hadi Makongorosi yenye zaidi ya kilometa 110 tayari imekamilika kwa asilimia 100.

Aidha, amebainisha kuwa maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kuanza ujenzi wa sehemu ya Doroto hadi Noranga yenye kilometa sita pamoja na kipande cha Itigi hadi Mkiwa chenye kilometa 25.

Amesema utekelezaji wa vipande hivyo viwili, vyenye jumla ya kilometa 31, utakamilisha sehemu ya Noranga hadi Mkiwa, huku kilometa takribani 356 zilizobaki zikiendelea kufanyiwa maandalizi ya kutafutiwa fedha na wakandarasi kwa ajili ya utekelezaji wake.

“Baada ya kukamilika kwa sehemu zote zilizopangwa, barabara hii yenye urefu wa kilometa 524 kutoka Mbeya hadi Mkiwa itakuwa imejengwa kwa kiwango cha lami,” alisema Mhandisi Nnko.

Mhandisi Nnko amesema barabara hiyo itakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kutokana na kupita katika maeneo yenye shughuli za kilimo, ufugaji na biashara mbalimbali, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.

Katika hatua nyingine, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kupitia Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara inayolenga kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi na kuimarisha maendeleo ya wananchi.