UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHA MSALATO WAFIKIA ASILIMIA 86
Dodoma, 28 Mei 2026
Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato unaendelea vizuri ambapo kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 86 kwa upande wa miundombinu inayotekelezwa na mkandarasi wa kwanza.
Mhandisi anayesimamia ujenzi wa kiwanja hicho kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mahona Luhende, amesema mradi huo unatekelezwa na wakandarasi wawili tofauti, ambapo mkandarasi wa kwanza ni Kampuni ya Sinohydro Corporation Limited anayehusika na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kiwanja hicho.
Amezitaja kazi zinazotekelezwa na mkandarasi huyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kutua na kupaa ndege (Runway) yenye urefu wa kilomita 3.6 na upana wa mita 60, pamoja na barabara mbili za ndege kuingia na kutoka katika maegesho ya ndege (Taxiways) zenye urefu wa mita 360 na upana wa mita 44.
Aidha, amesema kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa maegesho ya ndege (Apron) yenye urefu wa mita 480 na upana wa mita 240, barabara kuu ya kuingilia kiwanjani yenye urefu wa kilomita tano, barabara za ndani ya kiwanja, maegesho ya magari yenye uwezo wa kuhudumia magari 500 kwa wakati mmoja, mifereji ya kuondosha maji ya mvua, uzio wa kuzunguka eneo la kiwanja wenye urefu wa kilomita 41, pamoja na usambazaji wa huduma za umeme, maji safi na mfumo wa majitaka.
Mhandisi Mahona amesema mkandarasi wa pili ni Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group anayehusika na ujenzi wa majengo mbalimbali ndani ya kiwanja hicho, ikiwemo jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege wenye urefu wa mita 56.2, jengo la zimamoto na uokoaji, majengo ya umeme pamoja na jengo la utabiri wa hali ya hewa.
Amesema hadi sasa utekelezaji wa kazi za majengo umefikia asilimia 74 huku ujenzi ukiendelea vizuri.
“Mkandarasi huyu amekamilisha kazi za msingi za majengo (structural works) kwa asilimia 100 na kwa sasa anaendelea na kazi za umaliziaji (finishing works) pamoja na ufungaji wa mitambo mbalimbali,” amesema Mhandisi Mahona.
Ameongeza kuwa kazi zinazoendelea ni pamoja na ufungaji wa madaraja ya abiria (Passenger Boarding Bridges), ambapo kati ya madaraja matano, manne tayari yamefungwa, pamoja na ufungaji wa lifti tisa na escalator 18 kati ya 22 zinazotarajiwa kuwekwa.
“Kazi nyingi zimekamilika na kwa sasa tupo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi huu mkubwa. Tunayo matumaini makubwa kwamba ifikapo mwezi Agosti mwaka huu 2026 tutakuwa tumefikia hatua nzuri zaidi,” amesema.Mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa taifa kwa kuongeza fursa za biashara, utalii, uwekezajina usafiri wa anga kutokana na ujio wa ndege kutoka mataifa mbalimbali duniani.