MIZANI YA BARABARA YATAJWA KUWA SILAHA DHIDI YA UHARIBIFU WA MIUNDOMBINU
Pwani, 25 Mei, 2026
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa magari ya mizigo kupita kwenye mizani ili kulinda miundombinu ya barabara na madaraja pamoja na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara nchini.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa mizani mkoani Pwani, Msimamizi Mkuu wa Mizani Mkoa wa Pwani, Mhandisi Nzige Chibwaye, amesema mizani ina jukumu kubwa la kudhibiti uzito wa magari ili kuzuia uharibifu wa miundombinu inayotumia gharama kubwa kujengwa na kutunzwa.
Amesema magari yanayobeba mizigo yenye uzito mkubwa kupita kiwango kinachoruhusiwa husababisha uharibifu wa barabara na madaraja jambo linaloongeza gharama za matengenezo na wakati mwingine kukata mawasiliano kati ya maeneo mbalimbali.
“Tunafanya kazi ya kulinda miundombinu yetu hasa barabara, madaraja pamoja na usalama wa watumiaji wengine wa barabara. Magari yanapozidisha uzito huathiri ubora wa miundombinu na kuleta hasara kubwa kwa taifa,” amesema Mhandisi Chibwaye.
Aidha, amewataka madereva na wamiliki wa magari kuhakikisha wanahakiki uzito wa mizigo yao kabla ya kuanza safari ili kuepuka ukiukwaji wa sheria za mizani na kusaidia kulinda vyombo vyao vya usafiri.
Kwa upande wake, mmoja wa madereva wa malori amesema baadhi ya madereva bado wamekuwa wakipakia mizigo kupita kiwango kinachotakiwa jambo ambalo ni hatari kwa barabara pamoja na usalama wa safari zao.
Katika maelezo yake, Mhandisi Chibwaye amesema mizani huangalia uzito wa jumla wa gari pamoja na uzito wa kila ekseli kwa kutumia mfumo wa kisasa wa upimaji unaorahisisha kazi na kuongeza ufanisi ukilinganisha na mifumo ya zamani.
Amesema mfumo huo hutumia teknolojia maalum inayopokea taarifa za uzito na kutoa matokeo yanayotambulika kisheria, hali inayosaidia kudhibiti ukiukwaji wa sheria kwa haraka na usahihi zaidi.
Mbali na hilo, madereva wametakiwa kuhakikisha magari yao yako katika hali nzuri kabla ya kuingia kwenye mizani, ikiwemo kuepuka changamoto kama pancha au uvujaji wa mafuta ambayo yanaweza kuathiri shughuli za upimaji.
Kuhusu adhabu, amesema ukiukwaji wa uzito wa jumla wa gari na uzito wa ekseli ni makosa tofauti yanayotozwa faini kwa mujibu wa sheria, huku madereva wakitakiwa kupunguza mzigo uliopitiliza kabla ya kuendelea na safari.
Hatahivyo, ametoa wito kwa madereva kujifunza na kuzingatia sheria pamoja na kanuni za mizani ili kusaidia kulinda miundombinu ya taifa na kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa barabara.