News

BILIONI 40 ZA TAA AFCON NI MAKADIRIO, GHARAMA HALISI ZITAJULIKANA BAADA YA ZABUNI – TANROADS

BILIONI 40 ZA TAA AFCON NI MAKADIRIO, GHARAMA HALISI ZITAJULIKANA BAADA YA ZABUNI – TANROADS

Dodoma, 24 Mei, 2026

Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Ephatar Mlavi, amesema makadirio ya matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 40 kwa ajili ya uwekaji wa taa za barabarani kuelekea mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) si gharama halisi ya mradi, bali ni makisio ya awali yatakayothibitishwa baada ya mchakato wa zabuni kukamilika.

Akitoa ufafanuzi kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS kuhusu maandalizi ya AFCON 2027, Mhandisi Mlavi amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza miradi ya miundombinu ya barabara katika majiji ya Dar es Salaam na Arusha, ili kuhakikisha usafiri unakuwa bora wakati wa mashindano hayo.

Amesema Arusha ina mahitaji makubwa zaidi ya miundombinu kutokana na uwanja wa mashindano kujengwa katika eneo ambalo hapo awali halikuwa na barabara za kutosha.

“Tunaboresha miundombinu ili wananchi na wageni waweze kufika uwanjani kwa urahisi,” amesema.

Mhandisi Mlavi ameongeza kuwa pamoja na ujenzi wa barabara, TANROADS imejipanga kuweka taa za barabarani kwa ajili ya kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara na watembea kwa miguu.

Amesisitiza kuwa kiasi cha shilingi bilioni 40 kilichotajwa ni makadirio ya awali na gharama halisi zitajulikana baada ya zabuni kukamilika kwa mujibu wa sheria za manunuzi ya umma.

Pia ametoa ufafanuzi juu yaulinganisho wa taa za barabarani na taa za majumbani, akieleza kuwa taa za barabarani hutumia mifumo maalumu yenye viwango vya juu vya usalama pamoja na milingoti ya kitaalamu, wakati taa za majumbani hazina mifumo hiyo.

Aidha, amewahakikishia Watanzania kuwa TANROADS inaendelea kutekeleza miradi yake kwa kuzingatia sheria, uwazi na weledi ili kuhakikisha maandalizi ya AFCON 2027 yanafanikiwa.