News

PARESO AIPONGEZA SERIKALI NA TANROADS KWA MIRADI YA BARABARA NA UPANUZI WA UWANJA WA NDEGE LAKE MANYARA

PARESO AIPONGEZA SERIKALI NA TANROADS KWA MIRADI YA BARABARA NA UPANUZI WA UWANJA WA NDEGE LAKE MANYARA

Dodoma, 21 Mei,2026

Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Arusha, Cecilia Pareso, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya ujenzi, hususan barabara na miundombinu ya usafiri wa anga.

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi bungeni jijini Dodoma Mei 21, 2026, Pareso amesema Serikali imeendelea kufanya kazi kubwa inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi kupitia ujenzi wa barabara za lami na maboresho ya miundombinu ya usafiri.

Amesema ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami umekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi katika maeneo mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kuzipa kipaumbele barabara za kimkakati zinazochochea shughuli za kiuchumi katika mikoa na wilaya.

Akitaja Mkoa wa Arusha kuwa miongoni mwa mikoa yenye mchango mkubwa katika sekta ya utalii, Pareso amesema kuna maandalizi ya michezo ya AFCON 2027, hivyo miundombinu ya barabara inapaswa kukamilika kwa wakati ili kuendana na mahitaji ya kimataifa ya Mkoa huo.

Amesema katika Wilaya ya Karatu kuna barabara muhimu zinazohudumiwa na TANROADS Tanzania kupitia Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, ambaye amepongezwa kwa kusimamia matengenezo ya mara kwa mara ya barabara hizo pamoja na kuhakikisha zinaendelea kupitika katika hali nzuri.

Pareso ametaja barabara za Makuyuni–Ngorongoro Gate, Karatu–Mbulu yenye urefu wa kilomita 75, pamoja na Njiapanda–Mang’ola–Lalago yenye urefu wa kilomita 129, akisema barabara hizo zina umuhimu mkubwa kiuchumi, kijamii na kiutalii kwa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Karatu.

Amesema Serikali imepanga kuboresha sehemu ya barabara kuelekea hospitali ya wilaya kwa urefu wa kilomita 5, hatua ambayo ameielezea kuwa inalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Aidha, Mbunge huyo ameipongeza Wizara ya Ujenzi chini ya Waziri Abdallah Ulega kwa usimamizi wa miradi hiyo, akisema utekelezaji wake unaonesha kuzingatiwa kwa mahitaji ya wananchi na dhana ya kuwahudumia kwa karibu ya 'Kazi na Utu'.

Katika sekta ya utalii, Pareso ameeleza pia kuridhishwa na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Lake Manyara, akisema mradi huo utachochea ongezeko la watalii wanaotembelea Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro kupitia eneo la Karatu.

Ameongeza kuwa eneo la Karatu lina shughuli kubwa za kilimo cha umwagiliaji, hasa uzalishaji wa vitunguu vinavyosafirishwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi, huku akibainisha pia uwepo wa utafiti wa kutafuta mafuta katika eneo la Ziwa Eyasi, jambo linaloweza kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.

Pareso amehitimisha kwa kutoa pongezi kwa Serikali kwa juhudi za kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga, akisisitiza kuwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Lake Manyara utachangia kwa kiasi kikubwa kukuza utalii na uchumi wa Mkoa wa Arusha kwa ujumla.