WANANCHI WA GAIRO WATOA SHUKRANI ZAO KUFUATIA UJENZI WA MADARAJA YA CHAKWALE NA NGUYAMI, WATOA OMBI LINGINE
Dodoma, 21 Mei,2026
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Lucy Kombani, ameishukuru Serikali kwa kuwapatia wananchi wa Wilaya ya Gairo madaraja ya Chakwale na Nguyami yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 24, huku akiomba kukamilishwa kwa ujenzi wa daraja la Matare linalounganisha maeneo ya Idibo kuelekea Kilindi mkoani Tanga.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Mei 21, 2026, Kombani amesema wananchi wa Gairo wanaendelea kunufaika na juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya madaraja, lakini bado kuna changamoto ya daraja la Matare ambalo limekuwa likiombwa kwa muda mrefu.
“Wananchi wa Wilaya ya Gairo wanashukuru kwa kupatiwa madaraja ya Chakwale na Nguyami yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 24. Sasa tuna daraja dogo sana la Matare linalounganisha Idibo na kuelekea Kilindi mkoani Tanga pamoja na kata nyingi za Gairo ambalo tumeliomba kwa muda mrefu. Ni lini Serikali itatukumbuka na kukamilisha ujenzi wa daraja hilo?” alihoji Kombani.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa madaraja katika maeneo yaliyokuwa na changamoto kubwa ya usafiri na usafirishaji.
Amesema madaraja mengi yenye changamoto tayari yamekamilika na kwamba barabara inayohusisha daraja la Matare ipo katika mpango wa kusanifiwa pamoja na daraja hilo.
“Barabara hiyo hivi sasa ipo katika mpango wa kusanifiwa pamoja na daraja hilo. Namuelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro kwenda kwenye eneo hilo ili wakati tunakamilisha usanifu, tuone mahitaji yaliyopo na tuweze kutengeneza daraja hilo kwa muda,” alisema Kasekenya.