SERIKALI IMEWACHUKULIA HATUA WAKANDARASI WANAOKIUKA MIKATABA YA UJENZI - ULEGA
Dodoma, 20 Mei, 2026
Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wakandarasi na washauri elekezi wanaokiuka masharti ya mikataba ya ujenzi ili kuhakikisha miradi ya miundombinu nchini inajengwa kwa ubora unaotakiwa na kukamilika kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 20, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Waziri Ulega amesema hadi sasa Wizara imechukua hatua madhubuti kwa baadhi ya wakandarasi wa miradi ya barabara ambao walishindwa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa mikataba waliyoingia na Serikali.
Ametaja miradi ambayo mikataba yake imesitishwa kuwa ni pamoja na barabara ya Ibanda–Kajunjumele pamoja na mradi wa Sengerema–Nyehunge kutokana na kutoridhisha katika utekelezaji wake.
Aidha, amesema wakandarasi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Nne pamoja na mradi wa barabara ya Tungamaa–Mkange wamepewa onyo baada ya kushindwa kutimiza masharti ya mikataba yao.
“Katika kuhakikisha ubora wa miundombinu na kuwezesha miradi kukamilika kwa wakati, Wizara itaendelea kuchukua hatua stahiki kwa wakandarasi na washauri elekezi wanaokiuka masharti ya kimkataba,” amesema Waziri Ulega.
Amesema sambamba na hatua hizo, Wizara imezielekeza taasisi zilizo chini yake kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha inayotolewa na Serikali inapatikana.