News

SERIKALI KUENDELEA NA UJENZI WA BARABARA ZA HARAKA NCHINI

SERIKALI KUENDELEA NA UJENZI WA BARABARA ZA HARAKA NCHINI

Dodoma, 20 Mei, 2026

Serikali imeendelea na maandalizi ya mpango kabambe wa usafiri wa haraka (Tanzania Expressway Master Plan) utakaosaidia kuwa na mwongozo wa kimkakati wa maendeleo ya barabara za haraka nchini kwa lengo la kuboresha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Hayo yameelezwa leo Mei 20, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema mpango huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) na unalenga kuweka ramani pamoja na mwongozo wa maendeleo ya barabara za haraka katika maeneo mbalimbali nchini. 

Waziri Ulega amesema sambamba na maandalizi hayo, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya Expressway ikiwemo mradi wa Kibaha–Chalinze–Morogoro wenye urefu wa kilomita 163.8 ambao kwa sasa uko katika hatua za kumpata mwekezaji kupitia mfumo wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Aidha, amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanza upembuzi yakinifu wa awali kwa miradi mingine ya Expressway ikiwemo barabara ya Nyerere kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere yenye urefu wa kilomita 12.49.

Miradi mingine inayotarajiwa kufanyiwa upembuzi yakinifu ni pamoja na barabara ya Mandela na Sam Nujoma kuanzia Mfugale Flyover (TAZARA) hadi Ubungo na Mwenge yenye urefu wa kilomita 11.52 pamoja na mradi wa KIA hadi Arusha wenye urefu wa kilomita 45.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amesema Serikali itaendelea kuimarisha ubora wa miradi ya ujenzi kwa kusimamia viwango vya kitaalamu na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakuwa imara, salama na yenye kudumu kwa muda mrefu.

Amesema pia Wizara itaendelea kuboresha utoaji wa huduma kupitia taasisi zake kwa kuzingatia weledi, uwazi na mahitaji ya wananchi huku ikihimiza taasisi hizo kubuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuongeza ushiriki wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.