SERIKALI YASAINI MKATABA WA UJENZI WA BARABARA YA NJIA SITA DODOMA–CHAMWINO IKULU
�� Bilioni 241 kutumika katika ujenzi
�� Utaratibu wa Sanifu na Jenga kutumika
Dodoma, 18 Mei, 2026
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa upanuzi wa barabara ya Dodoma Mjini–Chamwino Ikulu yenye urefu wa kilometa 32 kuwa ya njia sita, mradi utakaogharimu takribani shilingi Bilioni 241 hadi kukamilika kwake.
Mkataba huo umesainiwa kati ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa niaba ya Serikali na China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) ya China, kwa lengo la kutekeleza upanuzi wa barabara hiyo kuwa ya njia sita.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa, jijini Dodoma Mei 18, 2026, Waziri Ulega ameiagiza TANROADS kuhakikisha inamsimamia mkandarasi huyo kwa karibu ili mradi huo ukamilike kwa viwango vya ubora vinavyolingana na hadhi ya jiji la Dodoma.
Ulega amesisitiza umuhimu wa kuwekwa kwa taa za kisasa, bustani, njia za watembea kwa miguu pamoja na miundombinu ya kuvutia, ili kuifanya Dodoma kuwa na sura ya jiji la kisasa.
“Tunataka mtu akipita usiku aione Dodoma inavyong’ara, taa za barabarani lazima ziwe za viwango vya juu,” amesisitiza Waziri Ulega.
Aidha, amewataka wataalamu wa usanifu kuzingatia usalama wa watumiaji wa barabara kwa kuweka maeneo salama ya kuvuka, hatua itakayosaidia kupunguza ajali zinazotokea katika baadhi ya maeneo ya jiji.
Vilevile, Ulega amebainisha kuwa sambamba na mradi wa DIST, Serikali tayari imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa ndani wa Jiji la Dodoma yenye urefu wa kilometa 6.4, unaofadhiliwa na Serikali ya Japan kwa gharama ya yen Bilioni 2.78.
“Lengo la mradi huo ni kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji na kurahisisha usafiri pamoja na shughuli za kijamii na kiuchumi katika makao makuu ya nchi,” amefafanua Ulega.
Kadhalika, ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya miundombinu kupitia ujenzi wa barabara na madaraja, kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za usafiri nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, aliyemwakilisha mkuu wa mkoa katika hafla hiyo ameishukuru Serikali kwa kutoa shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha utekelezaji wa mradi huo, huku akiahidi ushirikiano wa karibu kutoka kwa uongozi wa mkoa katika kipindi chote cha utekelezaji.
Shekimweri pia ameiomba Wizara kuzingatia zaidi usalama wa wananchi kwa kujenga vivuko vya juu au chini ya barabara, pamoja na kufunga kamera za usalama barabarani.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso, ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo, huku akiishauri kuendelea kutoa kipaumbele kwa miradi viporo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema mradi huo utatekelezwa kwa utaratibu wa Sanifu na Jenga (Design and Build), na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36, ikijumuisha miezi sita ya usanifu na miezi mitatu ya maandalizi ya awali.