News

MTENDAJI MKUU TANROADS ARIDHISHWA NA MRADI WA UBORESHAJI WA BARABARA YA BABATI–GEHANDU

MTENDAJI MKUU TANROADS ARIDHISHWA NA MRADI WA UBORESHAJI WA BARABARA YA BABATI–GEHANDU

Manyara, 17 Mei,2026

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, leo Mei 16, 2026 ametembelea mradi wa uboreshaji wa Barabara ya Babati–Gehandu unaosimamiwa na Ofisi ya Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara.

Katika ziara hiyo, Mhandisi Besta amekagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo na kujiridhisha na hatua inayofikiwa katika matengenezo ya barabara hiyo muhimu kwa shughuli za kiuchumi nchini.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mhandisi Besta amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha barabara yote inaboreshwa na kupitika kwa urahisi wakati wote.

“Lengo la mradi huu ni kuhakikisha barabara yote inabadilika na kupitika vizuri,” alisema Mhandisi Besta.

Mradi huo wa matengenezo ya Barabara Kuu ya Babati–Gehandu, ambayo ni kiungo muhimu cha uchumi wa nchi, unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.6 katika awamu ya kwanza, ambapo kilometa 15 zinatarajiwa kukamilika kabla ya kuendelea na hatua nyingine za uboreshaji.

Aidha, Mhandisi Besta alimesema Serikali kupitia Mfuko wa Barabara imetenga zaidi ya shilingi bilioni 20 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye changamoto mbalimbali nchini.

Pia amewahakikishia wananchi na watumiaji wa barabara hiyo kuwa kazi ya uboreshaji haitasimama, bali itaendelea kwa awamu mbalimbali huku ikitengewa fedha katika bajeti zijazo za Serikali.

“Kazi hii ni endelevu na hata mwaka ujao wa fedha barabara hii itaendelea kutengewa bajeti,” alisisitiza.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya kizawa ya Saimoo Company Ltd, ambayo ndiyo mkandarasi anayeshughulikia utekelezaji wa kilometa 15 za awali.

Kwa upande wake, mkandarasi huyo amewahakikishia wananchi kuwa kazi ya matengenezo inaendelea vizuri na kwamba katika kipindi kifupi kijacho kilometa 15 za mwanzo zitakuwa zimekamilika.

Vilevile, mkandarasi amemhakikishia Mtendaji Mkuu wa TANROADS kuwa viwango vya ubora vitazingatiwa katika utekelezaji wa mradi huo maalumu wa matengenezo ya barabara.