MIRADI AMBATISHI YAIBADILISHA KIGOMA, WANANCHI WANUFAIKA
Kigoma, 17 Mei,2026
Wananchi wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama kupitia miradi ambatishi inayotekelezwa na Wakala ya Barabara Tanzania TANROADS
Miradi hiyo inayotekelezwa katika maeneo ya Buhingwe–Beranka pamoja na Kidigwa imelenga kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na miradi ya barabara wanapata huduma muhimu za kijamii zitakazogusa maisha yao moja kwa moja.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Elisony Mweladzi amesema kuwa serikali imefanikiwa kujenga matanki mawili makubwa yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni moja za maji kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa maeneo hayo.
Amesema mkandarasi alianza utekelezaji wa mradi huo mwezi Julai mwaka jana na amefanikiwa kuukamilisha kwa asilimia 100 ndani ya muda uliopangwa, huku huduma ya maji ikiwa tayari imeanza kutolewa kwa wananchi.
“Kwa sasa maji tayari yamefika kwenye matanki na wananchi wameanza kupata huduma. Lengo letu ni kuhakikisha maeneo yote ambayo miradi ya barabara inapita, wananchi wake pia wanapata manufaa kupitia miradi ambatishi,” amesema Mweladzi.
Aidha, amesema mradi huo wa maji unatarajiwa kuhudumia vijiji vyote vya Buhingwe pamoja na maeneo jirani ya Manyovu, hatua ambayo itaondoa changamoto ya ukosefu wa maji iliyokuwa ikiwasumbua wananchi kwa muda mrefu hasa kipindi cha kiangazi.
Mbali na miradi ya maji, Kaimu Meneja huyo amesema serikali kupitia TANROADS inaendelea kutekeleza miradi mingine ya kijamii ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali pamoja na masoko ili kuinua maisha ya wananchi wanaozunguka maeneo ya miradi ya miundombinu.
“Tunawaomba wananchi waendelee kuitunza miundombinu hii kwa sababu serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha huduma hizi zinapatikana. Pia tunaendelea kusikiliza changamoto zao ili miradi inayotekelezwa iweze kuwagusa moja kwa moja,” ameongeza.
Kwa upande wake, mwananchi wa kijiji cha Buhingwe, Bwana Yoshua lindiga amesema kabla ya utekelezaji wa mradi huo wananchi walikuwa wakikumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, lakini sasa hali imebadilika na wananchi wameanza kupata huduma ya maji ya uhakika wakati wote wa kiangazi na masika.
Amesema mradi huo umekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo kwani umerahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi huku ukipunguza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.