News

ONE STOP BORDER KUFUNGUA FURSA ZA BIASHARA KIGOMA NA BURUNDI

ONE STOP BORDER KUFUNGUA FURSA ZA BIASHARA KIGOMA NA BURUNDI

Kigoma, 14 Mei,2026

Ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Manyovu (One Stop Border Post) kilichopo mpakani mwa Tanzania na Burundi unatajwa kuwa mkombozi mkubwa wa shughuli za usafirishaji, biashara na usafiri katika Mkoa wa Kigoma na nchi jirani ya Burundi.

Kituo hicho kinachosimamiwa na Wakala ya Barabara Tanzania, (TANROADS), kinatarajiwa kurahisisha huduma zote za forodha kufanyika eneo moja na hivyo kuondoa changamoto ya ucheleweshaji na usumbufu uliokuwa ukiwakabili wasafiri na wafanyabiashara wanaovuka mpaka huo.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Elisony Mweladzi, amesema kuwa mradi huo unaendelea vizuri huku mkandarasi akifanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Amesema mradi huo ulianza mwezi Julai mwaka jana na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu, ambapo hadi sasa maendeleo ya utekelezaji wake yanaridhisha.

“Progress ya mkandarasi ni nzuri, anaendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati. Tunaendelea kusisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji kwani vifaa na wataalamu wa kutosha wapo eneo la mradi,” amesema Mhandisi Mweladzi.

Mbali na ujenzi wa kituo hicho, mradi huo pia unahusisha ujenzi wa zaidi ya kilomita nne za barabara pamoja na daraja la kisasa litakalowezesha magari mengine kupita juu na mengine chini kwa urahisi zaidi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mweladzi , amesema kukamilika kwa kituo hicho kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Kigoma na Burundi kwa kuwa huduma zote za forodha zitakuwa zikifanyika sehemu moja na hivyo kurahisisha safari na biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa upande wake, Mhandisi wa eneo la ujenzi kutoka kampuni ya mkandarasi, Mhandisi Eradius Raphael, amesema kuwa ndani ya miezi miwili iliyobaki watahakikisha kazi zote zinakamilika kama ilivyopangwa.

Aidha, ameiishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo mkubwa akieleza kuwa utasaidia kuchochea maendeleo ya wananchi wa  Kigoma na maeneo mengine.