TANROADS KATAVI YASISITIZA MATUMIZI YA MIZANI KULINDA BARABARA
Katavi
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Katavi imesema itaendelea kusimamia matumizi ya mizani katika barabara kuu na za mikoa ili kudhibiti magari yanayobeba mizigo kupita kiwango kinachoruhusiwa,hatua inayolenga kulinda miundombinu ya barabara dhidi ya uharibifu wa mapema.
Akizungumza kuhusu hali ya barabara na shughuli za mizani mkoani humo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi Mhandisi Martin Mwakabende amesema,mkoa huo unahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 1,200 zikiwemo barabara kuu na za mikoa,pamoja na vituo viwili vya mizani vilivyopo katika barabara kuu.
Amesema mzani wa kwanza upo katika barabara kuu ya Tunduma - Sumbawanga - Mpanda - Uvinza kuelekea Kigoma katika eneo la Mugolokani lililopo kati ya Mpanda na Sitalike.Katika mzani huo hupimwa wastani wa magari 70 hadi 80 kwa siku,magari 500 hadi 600 kwa wiki na zaidi ya magari 3,000 kwa mwezi.
Aidha amesema,mzani wa pili upo katika eneo la Kamsisi wilayani Inyonga kwenye barabara kuu inayoelekea Tabora ambapo hupimwa wastani wa magari 130 kwa siku,magari kati ya 650 hadi 800 kwa wiki na kati ya magari 3,400 hadi 4,000 kwa mwezi.
Mhandisi Mwakabende amesema mikoa ya Katavi,Rukwa na Songwe ni maeneo makubwa ya uzalishaji wa mazao ya chakula ikiwemo mpunga na mahindi ambayo husafirishwa kwenda Tabora,Kigoma pamoja na nchi jirani za Burundi,Rwanda na Uganda.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha sheria za uzito zinazingatiwa TANROADS hutumia pia mizani inayohamishika(mobile weighbridge) kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika maeneo yenye viashiria vya uwepo wa magari yanayobeba mizigo kupita kiwango kinachoruhusiwa.
“Barabara nyingi zinajengwa kwa matarajio ya kudumu kwa miaka 10 hadi 20 lakini kuruhusu magari yenye uzito mkubwa kupita kiasi kunaweza kusababisha barabara kuharibika ndani ya miaka michache na kuongeza gharama za matengenezo kwa Serikali,”amesema.
Kutokana na hali hiyo Mhandisi Mwakabende ametoa wito kwa wasafirishaji wote ndani na nje ya Mkoa wa Katavi kuendelea kuheshimu viwango vya uzito vilivyowekwa ili kusaidia kulinda miundombinu ya barabara na kuhakikisha usafirishaji unakuwa salama na endelevu.