TANROADS IRINGA YABORESHA MIFUMO YA MIZANI KUPUNGUZA FOLENI NA KUENDANA NA ONGEZEKO LA MAGARI
Iringa, 01 Mei, 2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Iringa imeboresha mfumo wa mizani kwa lengo la kupunguza foleni na kukabiliana na ongezeko la magari, hatua inayoongeza usalama na ufanisi wa usafiri katika barabara kuu ya TANZAM.
Akizungumzia maboresho hayo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Hosea Machaka, amesema mkoa huo una jumla ya mizani sita katika vituo viwili vya Wenda na Kihorogota pamoja na mzani wa kubebeka (portable weighbridge) kwa ukaguzi wa kushtukiza.
Ameeleza kuwa Kituo cha Wenda kina mizani minne, ikiwemo miwili ya kudumu na miwili ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo (weigh-in-motion) huku Kihorogota ikiwa na mzani mmoja wa kudumu katika barabara ya Iringa–Dodoma.
Kwa mujibu wa Machaka, kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2025/2026 kumekuwa na ongezeko la magari zaidi ya 1,700, hali iliyosababisha msongamano mkubwa, hususan katika Kituo cha Wenda. Hata hivyo, changamoto hiyo imedhibitiwa kupitia maboresho ya mizani ya weigh-in-motion pamoja na kuanzishwa kwa njia mbadala kwa magari madogo yasiyohusika kupimwa.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kitengo cha Mizani, Mhandisi James Mziray, amesema magari yote yenye uzito kuanzia tani 3.5 yanapaswa kupimwa kwa mujibu wa Sheria ya udhibiti uzito ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.
Mhandisi Mziray Amefafanua kuwa dereva anapoingia katika mzani anatakiwa kuwa na nyaraka muhimu ikiwemo leseni halali ya udereva, kadi ya gari pamoja na nyaraka za mzigo husika kwa ajili ya ukaguzi, na endapo atakosa hataruhusiwa kuondoka hadi atakapowasilishiwa nyaraka hizo kwa njia ya mtandao.
Naye Msaidizi wa Msimamizi wa Kitengo cha Mizani, Bwana Felisian Kaizilege, amesema matumizi ya mizani ya weigh-in-motion yameongeza ufanisi kwa kupunguza muda wa upimaji na kuondoa foleni, akisisitiza madereva kuzingatia alama za taa ili kudumisha mtiririko mzuri wa magari na kuepusha msongamano.
Kaizilege amesisitiza umuhimu wa madereva kuzingatia alama za taa katika mizani hiyo, akibainisha kuwa taa nyekundu inaashiria gari kuingia kupimwa, huku taa ya kijani ikiruhusu kuendelea na safari ili kudumisha mtiririko mzuri wa magari na kuepusha msongamano usio wa lazima.