Serikali imeanza usanifu kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami itayounganisha Mikoa ya Simiyu, Singida, Manyara na Arusha ili kupunguza umbali wa safari uliopo sasa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa amesema barabara inayoanzia Meatu kupitia daraja la Sibiti hadi Singida, Hanang, Hydom, Mbulu, Karatu hadi Arusha litakapokamilika litapunguza Kilomita mia tano zinazotumika sasa na hivyo kuwapunguzia wananchi gharama na muda wa usafiri.
“Tumejipanga kuhakikisha ukanda wa Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida na Simiyu unaunganishwa kwa lami kwa njia fupi ili kuchochea uzalishaji wa mazao, kukuza utalii na uchumi wa mikoa hii” amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa amesema ujenzi wa barabara hiyo utahusisha daraja la Sibiti linalounganisha Mkoa wa Simiyu na Singida na barabara wezeshi za Hydom hadi Dongobesh na Mbulu hadi Mbuyu wa Mjerumani na hivyo kufungua ukanda wa mikoa ya kaskazini na kanda ya ziwa.
“Hakikisheni mnasimamia wakandarasi kikamilifu kwani sasa hivi mkandarasi akishasaini mkataba anapewa na fedha za kuanza ujenzi” amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Naye Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Maasay na Mbunge wa Mbulu Mjini, Zackaria Isaya wamesema kuwepo kwa barabara za lami kwa Wilaya ya Mbulu na Karatu kutachochea uzalishaji wa mazao ya kilimo na utalii na hivyo kuiwezesha wilaya hizo kuwa na uchumi imara.
Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa amesema Tanroads imejipanga kikamilifu kuhakikisha barabara za Wilaya ya Mbulu zinafunguka kwa kiwango cha Lami na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano pale watakapotakiwa kupisha baadhi ya maeneo kwa ajili ya ujenzi huo.
“Tumejipanga kuhakikisha kuwa barabara ya Katesh-Hydom-Mbulu hadi Karatu inasimamiwa kikamilifu na pale inapobidi kuipitisha pembezoni mwa mji ili kuepuka ulipaji mkubwa wa fidia na hivyo kuwezesha kazi kwenda kwa haraka” amesisitiza Mhandisi Rwesingisa.
Naibu Waziri Kwandikwa yuko katika ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu katika Mikoa ya Manyara na Arusha.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano