News

NW KWANDIKWA AWATAKA TANROADS ARUSHA KUSIMAMIA MIRADI IKAMILIKE KWA WAKATI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa amempa miezi tisa Mkandarasi Hanil-Jiangsu Joint Venture limited anaejenga barabara ya Mchepuo ya Arusha (Arusha Bypass) kukamilisha ujenzi huo.

Akizungumza mara baada ya kukagua barabara hiyo Mhe. Kwandikwa amesema kasi ya ujenzi huo iendane na ubora kama ilivyokuwa katika barabara ya awali ya Sakina-Tengeru KM 14.1.

“Hakikisheni ubora wa barabara hii pamoja na madaraja yake unawezesha magari ya aina zote kupita ili yasiingie katikati ya jiji na hivyo kutimiza azma ya Serikali ya kupunguza msongamano katikati ya jiji la Arusha’ amesema Mhe. Kwandikwa.

Naibu Waziri Kwandikwa amesema barabara hiyo licha ya kuwa na umuhimu mkubwa wa kibiashara katika jiji la Arusha na ukanda wa kaskazini pia itaungana na barabara ya Simanjiro- Kiteto hadi Kongwa na hivyo kuliunganisha jiji la Arusha na Makao Makuu ya nchi Dodoma.

Msimamizi wa mradi wa Arusha Bypass, Mhandis Sunday Boaz Lukumayi amemhakikishia Naibu Waziri kuwa malekezo yake yatasimamiwa kikamilifu na TANROADS Arusha ili barabara hiyo ikamilike kwa wakati.

Zaidi ya shilingi bilioni 139 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha madaraja saba.

Ujenzi wa Barabara ya Mchepuo ya Arusha (Arusha Bypass) yenye urefu wa Kilomita 42.4 ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kupunguza msongamano katika jiji la Arusha ili kuvutia watalii na kukuza uchumi wa jiji hilo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu-Loliondo sehemu ya kwanza ya Wasso- Sale Junction KM 49 na kumtaka Mkandarasi anaejenga barabara hiyo Kampuni ya China WU YI co. ltd  kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo chini ya miezi 24.

Amemtaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Arusha kuhakikisha Mkandarasi anapata Kokoto katika eneo lililo ndani ya mradi ili kuongeza kasi ya ujenzi huo.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha barabara ya Mto wa Mbu-Loliondo na Loliondo-Serengeti inajengwa kwa kiwango cha lami ili kuhuisha fursa za uchumi kwa wakazi wa eneo hilo na kuvutia biashara ya utalii.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Rashid Mfaume Taka amesema Wilaya yake imejipanga kikamilifu kupokea mradi mkubwa wa ujenzi wa lami na itatoa ushirikiano wa kutosha kwa mkandarasi ili kuhakikisha usalama na rasilimali watu unazingatiwa wakati wote wa mradi.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano