News

WAZIRI KAMWELWE ATOA SIKU SABA KWA MHANDISI MSHAURI KUPELEKA KAZI TANROADS

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, atoa siku saba kwa mhandisi mshauri kutoka kampuni ya Studi International aliyefanya usanifu wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato mjini Dodoma,  kukabidhi nyaraka za usanifu huo kwa Wakala wa Barabara (TANROADS).

Mhandisi Kamwelwe ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam, alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua hatua za maendeleo ya ujenzi wa jengo la tatu la abiria ambapo pamoja na mambo mengine amewataka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), kuendelea kusimamia uendeshaji wa viwanja na si kujihusisha na ujenzi.

"Wale wote ambao wameingia mkataba na wanaotarajia kuingia mkataba wanatakiwa kuwasilisha mikataba hiyo TANROADS  na sio TAA kama awali kutokana na muundo mpya uliowekwa hivi sasa", amesema Mhandisi Kamwelwe.

Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, Waziri Mhandisi Kamwelwe, ameridhishwa na kasi ya ujenzi wake ambapo mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia zaidi ya 78 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Mei Mwakani.

Ameongeza kuwa kutokana na kuongezeka shughuli za kibiashara na idadi ya abiria katika uwanja huo Serikali iliamua kujenga jengo la tatu la abiria litakalokuwa na uwezo wa kubeba abiria milioni sita kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya abiria wanaotumia  usafiri wa anga.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Julius Ndyamukama, amemuhakikishia Waziri Kamwelwe kumsimamia mkandarasi anayejenga jengo hilo kukamilisha kwa wakati na kukidhi viwango vya kimataifa.

Mhandisi Ndyamukama, amesema mpaka sasa Mkandarasi hadai fedha yoyote na mradi utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 564.

Jengo la kwanza la abiria  lilijengwa mwaka 1956 na lilikuwa na uwezo wa kuhudumia abiria laki tano kwa mwaka wakati jengo la pili la abiria lilijengwa mwaka 1984 na lina uwezo wa kuhudumia abiria  milioni moja na nusu kwa mwaka.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano