News

SERIKALI KUWEKEZA KWENYE HANGA KATIKA KIWANJA CHA NDEGE CHA KIA

Serikali imesema kuwa itaanza kukarabati karakana (hanga) iliyopo Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), ili ndege zote zilizonunuliwa ziweze kutengenezwa hapa nchini na kuwa ya mfano kwa Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.


Amezungumza hayo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, katika kiwanja cha ndege cha KIA alipokuwa akikagua jengo lililopo katika karakana hiyo na kumtaka mkandarasi atakayepewa kazi ya kukarabati amalize ndani ya miezi mitatu kwa kuwa kazi hiyo si kubwa.


"Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Shirika la Ndege halifi hivyo tutakarabati hii karakana ili kuwezesha miundombinu wezeshi kwa ndege zetu", amesema Mhandisi Kamwelwe.

 

Amefafanua kuwa kukamilika kwa usimikaji wa  vifaa maalumu katika karakana hiyo (hanga) na ukarabati wa jengo lenye vyumba mbalimbali kwa ajili ya kutolea mafunzo ya vitendo kutaongeza tija kwa Shirika na kutimiza  lengo la Baba wa Taifa la kuifanya kuwa karakana yenye uwezo mkubwa wa kutoa mafunzo ya vitendo kwa mafundi, wahandisi, marubani, wasaidizi wa ndege kwani rasilimali zote zitapatikana.

 

Waziri Kamwelwe  ameendelea kueleza kuwa sasa ni wakati hata wa vyakula vinavyotolewa kwenye ndege kutengenezewa katika mgahawa uliopo katika karakana hiyo badala ya kuchukua chakula kutoka  kwa watoa huduma wengine.

 

Aidha amemtaka Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege nchini (ATCL), kusimamia shirika hilo kikamilifu ili liweze kujiendesha kwa faida na kutafuta vyanzo vingine vya kuongeza mapato ya shirika na sio kutegemea ukataji wa tiketi tu.

 

Waziri Mhandisi Kamwelwe, ameongezea kuwa ukarabati huo utaenda sanjari na ukarabati wa nyumba zaidi ya 30 za watumishi  ambapo zikikamilika  zitatumiwa kama makazi kwa marubani na mafundi wa ndege ili kuwawezesha kuwa karibu hususan wakati wa dharura.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege nchini (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi, amesema kuwa mpaka sasa wametenga kiasi cha shilingi milioni 500 na gharama halisi za ukarabati wa karakana hiyo zaidi ya Shilingi milioni 600.

 

Ameongeza kuwa shirika limejipanga vyema kufufua karakana hiyo kwa kuanza na ukarabati wa mfumo wa umeme na kupaka rangi maalumu katika vyumba vya mafunzo na kununua vifaa vya kutolea mafunzo hayo ikiwa  na lengo la kuwaongezea uwezo mafundi wetu kwa ajili ya kutengeneza ndege zetu.

 

Waziri Kamwelwe yupo mkoani arusha katika ziara ya kikazi ya kukagua viwanja vya ndege na kuona hali ya miundombinu yake.