News

UJENZI WA KITUO CHA UKAGUZI WA PAMOJA MANYONI KUKAMILIKA SEPTEMBA MWAKA HUU

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Kituo cha Ukaguzi wa Pamoja (One Stop Inspetion Station-Osis) kinachojengwa Wilayani Manyoni, Mkoani Singida  na Kampuni ya Impresa di Costruczioni Ing. E. Mantovan S.p.a con socio unico Via Belgio ya nchini Italia na kusema kuwa kukamilika kwake kutarahisisha uchukuzi katika nchi za ukanda wa kati.

Akizungumza Mkoani mkoani humo mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo Naibu Waziri Kwandika amesema mradi huo ni utekelezaji wa maazimio ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kupunguza ucheleweshaji wa huduma za uchukuzi kwa njia ya barabara hususani kwa mizigo inayoelekea nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

“Niwapongeze kwa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi huu kwani kukamilika kwa mradi huu, kutapunguza sana muda unaopotezwa na madereva wanaosafirisha mizigo na nje ya nchi sababu kwa sasa wanakaguliwa kwenye vituo zaidi ya 30 nchini” amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Naibu Waziri Kwandikwa ameongeza utawaweka pamoja wadau pamoja wakiwemo Wakala wa Forodha (TRA), Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Jeshi la polisi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa muda mfupi.

Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa amewataka wananchi wa Wilaya ya Manyoni kutumia fursa ya uwepo wa kituo hicho kwa kuanza kujenga sehemu za huduma ya chakula ili  kupitia uwekezaji huo wapate kipato na kuinua uchumi wao, Wilaya na Mkoa kwa ujumla.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Singida, Eng. Leonard Kapongo, amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa atamsimamia  mkandarasi huyo na kuhakikisha kasi inaendana na viwango vilivyopo kwenye mkataba ili mradi ukamilike kwa wakati.

Naye Mhandisi Mkazi Kutoka Kampuni ya NIMEA Consult (T) ltd, Eng. Patrick Lutinya, amesema ujenzi wa kituo hicho kwa sasa umefikia asilimia 45 na kumhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa hawataomba muda wa ziada wa utekelezaji wa mradi huo na watahakikisha unakamilika kwa wakati kama mkataba unavyosema.

Mradi wa Kituo cha Ukaguzi wa Pamoja (One Stop Inspetion Station-Osis), utagharimu takribani kiasi cha euro bilioni 9 na unatarajiwa kukamilika mwezi septemba mwaka huu.

Imetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kitengo cha Mawasiliano Serikali.