News

WANAWAKE WAASWA KUCHANGAMKIA KAZI ZA BARABARA

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imesema itahakikisha wanawake walio katika Sekta ya Uhandisi na Ukandarasi wanapata fursa za kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na matengenezo ya barabara.

 

Hatua hii inalenga kuongeza ushirikishwaji wa wanawake katika sekta hiyo ili kufikia lengo la kuwa na uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume ifikapo mwaka 2025.

 

Akizungumza mkoani Morogoro, wakati wa ufungaji wa semina elekezi kwa waratibu wa mikoa wa ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara kutoka ofisi za Wakala wa Barabara (TANROADS), mikoa yote Tanzania bara, Mkuu wa Chuo cha Ujenzi, Morogoro Bw. Melkzedeck Mlyapatali, amewashauri kuwa mabalozi wazuri wa kuwahamasisha na kuelimisha wanawake katika maeneo yao ya kazi kuchangamkia fursa hizo.


Aidha amewaasa waratibu hao kuhakikisha wale wanawake ambao tayari wamefanikiwa kupata kazi  hizo zifanywe kwa kuzingatia ubora, gharama nafuu na kuzingatia muda uliopangwa kwenye mkataba.


Bw. Mliyapatali ametumia fursa hiyo kutoa wito na kuwahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao hususan wa kike katika Vyuo vya Ufundi ili kupata ujuzi wa masuala ya Ujenzi utakaosaidia kuondoa dhana kuwa masomo ya ufundi ni kwa ajili ya watoto wa kiume tu.


"Mimi pia ni mwalimu hapa chuoni, kwa uzoefu wangu nimegundua kuwa ukimfundisha mtoto wa kike anakuwa mahiri na weledi wa hali ya juu, tofauti na mtoto wa kiume", amesema Bw. Mlyapatali.


Kwa upande wake Mratibu wa kitengo cha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Rehema Myeya, amewahimiza waratibu walioshiriki semina hiyo kutoka Mikoa mbalimbali kuwa chachu ya maendeleo katika vituo vyao vya kazi na kuhakikisha kuwa wanawake watakaopata kazi za ujenzi au matengenezo ya barabara zinakuwa katika viwango vinavyokubalika.


Naye Mratibu kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Prisilla Mushi, ameahidi kusimamia, kuelimisha, kuhamasisha na kutoa msukumo kwa jamii katika ushiriki wa wanawake kwa kutumia teknolojia katika kazi za barabara.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano