News

WANAWAKE KUPEWA KIPAUMBELE MIRADI YA UJENZI

WANAWAKE  KUPEWA KIPAUMBELE  MIRADI  YA UJENZI

Uwiano wa wanawake katika miradi mingi ya ujenzi nchini ikiwemo matengenezo na usimamizi wa barabara unaelezwa kufikia asilimia 6 na 7 kati ya wahandisi 100 ukilinganisha na wanaume katika Sekta ya hiyo.

Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara(TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses Kiula, wakati akifungua semina elekezi kwa waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara nchini na kufafanua kuwa hali hiyo inatokana na ushirikishwaji mdogo wa wanawake katika kazi hizo.

Aidha, Mhandisi Kiula,  amesisitiza umuhimu wa semina hiyo kwa waratibu hao ili kuwajengea uwezo, ujuzi na njia mbadala za kuongeza idadi ya wanawake watakaoshiriki katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara na pia  kuhamasisha wanawake wengine zaidi kushiriki kazi hizo.

"Serikali sasa inalenga kuwawezesha makadarasi wanawake kufikia madaraja ya juu ya ukandarasi ili kuweza kuinua kipato chao na kuondokana na umasikini katika familia na jamii kwa ujumla", amesisitiza Mhandisi Kiula.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo elekezi yatawasaidia katika kupambanua masuala muhimu yatakayoweza kurahisisha uratibu na usimamizi mzuri katika utendaji wa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara kwa ufanisi zaidi.

"Ni maratajio yangu mkimaliza mafunzo haya mtatekeleza kazi zenu kwa ufanisi zaidi na kuleta matokeo chanya  kwa jamii na Taifa", amesema Mhandisi Kiula

Kwa upande wake Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Rehema Myeya, amesema kuwa kazi kuu za waratibu hao ni kuwahamasisha wanawake kushiriki kwa wingi katika kazi za barabara katika mikoa yote ili kutanua wigo wa maendeleo katika jamii na mafanikio katika kazi hizo. 

Mhandisi Myeya, ametaja mada zitakazojadiliwa katika semina hiyo kuwa ni masuala ya jinsia na namna ambavyo Serikali inayashughulikia ikiwemo sheria ya ujenzi na namna inavyosisitiza ushiriki wa wanawake na kuipitia sheria ya manunuzi na kuona maeneo ambayo yanatoa kipaumbele kwa wanawake.

Mada nyingine ni kuangalia mchakato wa usajili kwa makampuni ya wanawake, kupitia mwongozo wa kuimarisha ushiriki wa wanawake katika kazi za barabara na masuala mtambuka, namna ya kuandaa zabuni ambazo zinaakisi mahitaji ya wanawake na ufanisi wa teknolojia ya nguvu kazi katika kufanya matengenezo ya barabara. 

Ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara kitaifa ulianza mwaka 1992 katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Shinyanga, Mwanza na Mtwara na hii ni kutokana na kazi hizo kufanywa na wanaume hasa kwenye nyanja za makandarasi na wahandisi washauri.