News

TANROADS YATAKIWA KUILINDA MIUNDOMBINU YAKE

Kamati ya Bunge ya Miundo mbinu imeutaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), kujipanga nakuja na mikakati bora ya kuilinda miundombinu ya barabara za lami inazozijenga hapa nchini ili ziwe fursa za kiuchumi badala ya kuwa chanzo cha ajali.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Sulemani Kakoso amesema  hayo mara baada ya kamati yake kutembelea ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Tabora KM 259 inayojengwa kwa kiwango cha lami na kusisitiza kuwa umefika wakati kwa TANROADS kutoa elimu kwa jamii za vijijini kuzilinda barabara zinazojengwa na kuzitumia fursa za uwepo barabara za lami kujiletea maendeleo.

“Hakikisheni mnakuwa na programu endelevu za kuwaelimisha wananchi umuhimu wa barabara za lami ili badala ya kuzihujumu kwa kuharibu miundombinu ya barabara hizo wazilinde na kuzitumia kuibua fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao”, amesema Mhe. Kakoso.

Akizungumza katika ziara hiyo Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anaeshughulikia sekta ya Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Serikali imejipanga kuufungua mkoawa Tabora kwa kuhakikisha unafikika kwa pande zote kwa barabara za lami ili kuhuisha fursa za uzalishaji na kukuza uchumiwa wananchi wake.

“Tumeigawa barabara hii katika sehemu tatu ili kuharakisha ujenzi wake ambapo sehemu ya Manyoni- Itigi- Chaya KM 89.5 na Tabora–Nyahua KM 85, ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika na sehemu ya Chaya-Nyahua KM 85.4 mkandarasi anaendelea na ujenzi”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Nae meneja wa TANROADS mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo na Tabora Eng. Damian Ndabalinze wameihakikishia Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuwa watatekeleza utoaji elimu ya matumizi bora ya barabara na kudhibiti maeneo yenye ajali nyingi katika mikoa yao ili jamii katika mikoa hiyo zinufaike na uwepo wa barabara za  lami.

Kamati ya Bunge ya Miundombinu iko katika ziara ya kutembelea miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma ili kujifunza na kushauri namna bora ya kuendeleza miundombinu hapa nchini na hivyo kuwezesha malengo ya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kutekelezeka.

Imetolewa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini