News

UJENZI WA BARABARA YA KIDATU-IFAKARA KUKUZA UCHUMI WA MOROGORO

Serikali imesema imeanza ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa KM 66.9 kwa kiwango cha lami ambapo kukamilika kwake kutachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika wilaya za mkoa wa Morogoro.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipokuwa akikagua maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo amemuagiza mkandarasi wa kampuni ya Reynolds Construction kutoka Nigeria anayejenga barabara hiyo kujenga kwa viwango na kukamilisha kwa wakati.

"Mradi huu umesuburiwa kwa siku nyingi na wananchi wa wilaya hii na mkoa kiujumla, mategemeo ya Serikali ni kuwa  mradi huu utaukamilisha mapema mwezi Aprili, 2020 kwa kuzingatia vipengele vya mkataba na kwa viwango stahiki", amesema Prof. Mbarawa.

Amesema kuwa  ujenzi katika  barabara hiyo unatarajiwa kuhusisha ujenzi wa madaraja makubwa mawili, madaraja madogo manne, makalvati makubwa na madogo 271 na unatarajiwa kudumu kwa miaka 20.

Aidha, Prof Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itahakikisha wananchi wa mkoa huo wanapewa kipaumbele kwenye ajira mara tu kazi itakapoanza ili kuongeza kipato chao.

"Mradi umeanza na nimemuelekeza mkandarasi kuajiri afisa mwajiri ili kuhakikisha nafasi nyingi za ajira zinapatikana kwa wazawa kwani nafasi 70 walizoajiri mpaka sasa ni za mwanzo tu, ila nafasi nyingine zitaongezwa", amefafanua Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. James Ihunyo, ameipongeza Serikali kwa jitihada inazozifanya kuboresha miundombinu ya barabara hapa nchini na amemuahidi Waziri Prof. Mbarawa kuwa wananchi na uongozi wa usalama wa Wilaya yake watatoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo ili waweze kunufaika na mradi huo mapema.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Dorothy Ntenga, amesema kuwa kazi halisi itaanza mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu na watahakikisha wanamsimamia mkandarasi kwa karibu ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na viwango.

Ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 kwa kiwango cha lami unatarajiwa kujengwa kwa miezi 30 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 111.4 na unafadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (European Union), Shirika la Misaada la Uingereza (UK aid) na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.