News

PROF. MBARAWA AWAONYA TBA.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, ameuagiza Wakala wa Majengo (TBA), kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miradi yote waliyopewa na Serikali kwa wakati. 

Prof. Mbarawa amesema hayo wakati akikagua ujenzi hospitali ya mkoa, makazi ya Mkuu wa Mkoa na nyumba za watumishi zinazojengwa na Wakala huo eneo la Nyaumata mjini Bariadi mkoani Simiyu, na kusisitiza kuwa ikiwa watashindwa kumaliza kwa wakati miradi yote kama mikataba inavyosema, Serikali haitatoa kazi ya ujenzi wowote kwa TBA. 

“Tunaamini TBA mnafanya kazi nzuri na kwa ubora, lakini kazi mnazopewa hazikamiliki kwa wakati, mkisikia viongozi tunakagua mradi ndio mnaanza kufanya kazi”, amesema Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa Serikali haiwezi kuendelea kuwapa miradi, wakati ujenzi wa miradi hiyo inasuasua, nakuwataka waongeze kasi, kuzingatia ubora na wakati kulingana na mikataba inavyosema.

Aidha ameonesha kutofurahishwa hata kidogo na malalamiko yanayotolewa na baadhi ya viongozi kuhusu wakala huo kushindwa kumaliza kwa wakati miradi wanayojenga. 

"Sifurahishwi na malalamiko na kasi ndogo iliyokuwa ikiendelea ya utekelezaji wa miradi sehemu mbalimbali ikiwemo baadhi ya miradi iliyopo kwenye mikoa ya Kigoma, Mara na Dar es Salaam, hali hii haikubaliki hata kidogo", amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, amesema kuwa mkoa umewapa TBA miezi mitatu kukamilisha miradi hiyo kwa viwango vinavyostahili na kwa wakati.

Awali akitoa maelezo ya miradi inayotekelezwa na TBA mkoani Simiyu, Meneja wa Wakala huo wa mkoa, Rick Maitale, amesema kuwa wanatekeleza miradi 10 ndani ya mkoa ambapo changamoto kubwa ni upatikanaji wa fedha kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ametembelea kambi ya mkandarasi wa kampuni ya CHICO kutoka China anayejenga barabara ya Maswa-Bariadi yenye urefu wa KM 49.7 kwa kiwango cha lami na kumuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani humo, Mhandisi Albert Kent, kuhakikisha barabara hiyo inakamalika ndani ya miezi 19 na thamani ya fedha na ubora unazingatiwa.

Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo utagharimu takribani kiasi cha shilingi bilioni 87 na unafadhiliwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano