News

SERIKALI YAMCHARUKIA MKANDARASI DOTT

Serikali imemtaka Mkandarasi Dott Services anayejenga barabara ya Mtwara-Mnivata yenye urefu wa KM 50 kwa kiwango cha lami kuongeza vifaa na kasi katika ujenzi wa barabara hiyo ili kurahisisha huduma za usafirishaji wa mazao na abiria kwa wananchi wa mkoa huo.

Akitoa agizo hilo mkoani Mtwara, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na kusisitiza kuwa mkandarasi huyo anatakiwa kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaendana sawia na thamani ya fedha zilizotolewa na ubora kwa kiwango cha kisasa.

"Hakikisha unaongeza vifaa na kasi ya ujenzi wa barabara hii, la sivyo tutakutoa na hutapata kazi nyingine ya ujenzi wa barabara hapa nchini", amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Ametoa rai kwa Makandarasi wote nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili, weledi na kuhakikisha kazi wanazopewa zinakamilika kwa wakati na ikiwezekana hata kabla ya muda wa mkataba ili kuweza kuokoa fedha za Serikali.

Aidha ameutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani hapo pamoja na Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Kyongdong Engineering, kuusimamia madhubuti mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyostahili na hivyo kuweza kufungua fursa za kiuchumi na maendeleo kwa mkoa huo haraka iwezekanavyo.

Naibu Waziri huyo amesema nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri na ya uhakika kupitia miundombinu bora ya barabara vipindi vyote vya mwaka hivyo fedha za kuwalipa makandarasi zipo tayari ni jukumu lao kuikamilisha mapema.

Naye Meneja wa TANROADS mkoani hapo, Mhandisi Dotto Chacha amemhakikishia Naibu Waziri huyo kumsimamia mkandarasi huyo na kuhakikisha anamaliza ujenzi wa barabara hiyo kama ilivyopangwa katika mkataba.

Kwa upande wake Mkandarasi anayejenga barabara hiyo Mhandisi Michael Mudanye, ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwalipa fedha za awali ambazo zimewasaidia kuleta vifaa eneo la kazi.

Ameongeza kuwa wamejipanga kukamilisha barabara hiyo kwa wakati kwani watafanya kazi usiku na mchana.

Mbunge wa Jimbo la Nanyamba mkoani humo, Mhe. Abdallah Chikota, amesema kuwa wananchi wanaisubiri barabara hiyo ikamilike kwa lami kwa kipindi kirefu kwani wamekuwa wakiteseka kutokana na vumbi pamoja na mashimo yaliyopo katika barabara hiyo.

Ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mnivata KM 50 utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 89 na unatarajiwa kukamilika mwezi January mwakani. Barabara hiyo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Mtwara-Newala-Masasi KM 210 kwa kiwango cha lami.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano