Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ameuagiza Uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) makao makuu kusaini haraka mkataba kwa mkandarasi atakayebeba kivuko kipya kutoka eneo kinapotengenezwa wilayani Pangani mkoani Tanga hadi mkoani Lindi.
Akizungumza mara baada ya kukagua maegesho ya kivuko hicho ambacho kinatarajiwa kutoa huduma za usafiri kutoka Lindi Mjini - Kitunda mkoani humo, Naibu Waziri huyo amewahakikishia wananchi kutegemea kupata huduma nzuri za usafiri kwani ujenzi wa kivuko na maegesho yake kwa sasa umefika katika hatua nzuri.
"Naagiza Mamlaka husika kusaini haraka mkataba kwa mkandarasi atakayebeba kivuko hiki kutoka Tanga hadi hapa ili wananchi waone kwamba kivuko kimefika na kipo tayari kwa ajili ya kutoa huduma", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameridhishwa na ujenzi wa maegesho hayo ambayo kwa sasa ujenzi wake umebakia asilimia 10 na hivyo kutarajiwa kukamilika muda wowote.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa, ametembelea na kukagua uwanja wa ndege wa Lindi ambapo amesema Serikali inaendelea na mpango wake wa kuboresha viwanja vya ndege nchini ili kuimarisha huduma katika usafiri wa anga.
Amefafanua kuwa Serikali kupitia mwaka wa fedha 2018/19 licha ya kuwa na mpango wa kuboresha uwanja huo pia itaboresha Uwanja wa ndege wa Kilwa Masoko lengo ni kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa TEMESA mkoani Lindi, Mhandisi Greyson Maleko, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kujipanga katika kuhakikisha wananchi wa Lindi wanapata huduma bora za kivuko.
Naye, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani humo Mheshimiwa Hamida Abdallah, ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusogeza maendeleo kwa wananchi na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.