Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mb), amewapongeza Wakala wa barabara nchini (TANROADS), kwa mikakati wanayotumia kudhibiti vitendo vya rushwa katika vituo vya mizani hapa nchini.
Akifungua Mkutano wa tisa wa baraza la wafanyakazi la TANROADS mjini Kigoma, Naibu Waziri Kwandikwa, amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha watendaji wake wote wanakuwa waadilifu ili rasilimali chache zitumike kwa manufaa ya wote.
“Hakikisheni kila mtakaye mkamata kwa vitedo vya rushwa hatua za kisheria anachukuliwa ikiwemo na kufukuzwa kazi ili kuonyesha kuwa jambo la rushwa tunalichukia na hatulipendi katika Serikali”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Naye Mtendaji Mkuu Wa Wakala huo Eng. Patrick Mfugale, amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja watumishi 71 wamefukuzwa kazi katika vituo mbalimbali vya mizani hapa nchini kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Ameongeza kuwa TANROADS wamejipanga kuhakikisha miradi yote ya ujenzi na vituo vya mizani vinafanya kazi kwa weledi na uaminifu ili kujenga imani kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TANROADS Hawa Mmanga, amemuhakikishia Naibu Waziri wa Ujenzi kuwa wakala wake umejipanga kutekeleza kikamilifu ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja hapa nchini kwa wakati, ubora na kuzingatia thamani ya fedha.
Wajumbe wa baraza la TANROADS kutoka mikoa yote nchini wamekutana katika mkutano wa tisa wa baraza la wafanyakazi ili kutathimini utendaji kazi wao na kuibua mikakati mipya itakayowezesha wakala huo kufanya kazi zake kwa weledi na kwa kukidhi mahitaji ya nchi.