News

PROF. MBARAWA AMCHARUKIA MKANDARASI WA SIA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ametoa miezi mitatu kwa mkandarasi GM Construction anayejenga jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA), kukamilisha ujenzi huo.

Amesema Serikali hairidhishwi na kasi ya ujenzi wa jengo hilo ambalo limetumia miaka minne badala ya miwili iliyokubalika katika mkataba wa awali hivyo kumtaka mkandarasi huyo kuhakikisha analikabidhi jengo hilo ifikapo Januari 30 mwakani.

“Kushindwa kukamilisha jengo hili ifikapo mwezi Januari mwakani itakuwa ndio tiketi yako ya mwisho ya kutopewa kazi kwasababu Serikali hii inafanya kazi kwa kuzingatia ubora na muda”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Mbeya Eng. Paul Lyakurwa kusimamia kikamilifu ujenzi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa

“Ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege kwa sasa unasimamiwa na TANROADS na uendeshaji wake unasimamiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuongeza kasi ya ujenzi wa viwanja vya ndege na ubora wa huduma zinazotolewa katika viwanja hivyo”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa, amekagua upanuzi wa barabara katika mji wa Tunduma unaolenga kupunguza msongamano wa magari katika eneo hilo na kuwahakikishia wananchi kuwa ujenzi wake utakamilika mwishoni mwa mwezi ujao.

Amewataka wakazi wa Tunduma kuilinda miundominu ya barabara hizo kwa kuzingatia matumizi sahihi ili kuleta usalama kwa wananchi.

Naye Meneja wa TANROADS, mkoa wa Songwe Eng. Yohane Kasaini, amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kwamba barabara za michepuko zitaongezwa katika eneo la Tunduma ili kurahisisha shughuli za kibiashara na uzalishaji katika mji huo.

Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miundombinu katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano