News

BARABARA YA TABORA HADI MPANDA YAKAMILIKA KWA KIWANGO CHA LAMI

Mhe Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, leo tarehe 18 Mei 2022 amefanya ufunguzi  rasmi wa barabara Tabora,  Koga hadi Mpanda yenye kilomita 342.9 iliyo kamilika kwa kiwango cha lami inayounganisha mikoa wa Katavi na Tabora.

Akiongea na wananchi mkoani Tabora, Mhe Rais aliwataka wananchi kuilinda barabara  hiyo lakini pia kufuata sheria zote za usalama zilizowekwa ili kuifanya barabara hiyo kudumu na kuongeza usalama wa watu na mali zao huku akisistiza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutapelekea kuongezeka kwa wawekezaji na kupanua uchumi kwenye ukanda huyo na nchi kiujumla.

Kwa upande wake Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, alisisitiza kukamilika kwa barabara hiyo kutahamasisha wananchi kufanya biashara za kitaifa na kimataifa kwa mfano  biashara kati ya Katavi, Tabora, Kigoma na nchi za jirani kupitia kusafirisha mazao ya kilimo” alisema.

Akitoa taarifa za mradi, Mhandisi Rogatus Mativila ,Mtendaji Mkuu wa TANROADS alisema barabara hii imejengwa na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) chini ya program ijulikanayo kama Transport Sector Support Program (TSSP) kwa ghamara ya bilioni 473.879 ambapo ujenzi ulianza Machi 18  mwaka 2018 na kukamilika Desemba 26 mwaka  2021.

Kwa upande wake Dkt. Patricia Laverley, Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo nchini Tanzania alisema “Barabara hii itaenda kusaidia kutatua tatizo la usafiri kwa watu na mizigo lakini sana sana zaidi barabara hii ni kiungo muhimu kwa programu ya maendeleo ya Tabora na Mpanda.”  

Aliongeza “Itahudumia maeneo ya Nyanda za Juu Kusini, Ukanda wa Ziwa, Ukanda wa Mashariki pamoja na maeneo mengine ya nchi hii.

Alimaliza kwa kusema barabara hii itakua kiunganishi muhimu kati ya nchi yetu na nchi kama Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia bandari ya Kasanga na mpakani Tunduma na Kasesha.