BODI YA KITUO CHA UMAHIRI WA USALAMA BARABARANI YAZINDULIWA RASMI
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, leo Alhamisi Septemba 18, 2025 ameongoza uzinduzi wa Bodi shirikishi ya Kituo cha Umahiri wa Usalama Barabarani (Regional Center of Excellence on Road Safety) katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam.
Ikumbukwe TANROADS kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wameanzisha kituo hicho kwa lengo la kuimarisha usalama barabarani nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, kwa kutoa mafunzo, kufanya tafiti, pamoja na kushauri serikali na jamii kuhusu mbinu bora za kuzuia ajali sambamba na kutekeleza maazimio ya kimataifa yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhandisi Besta amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni hatua muhimu katika kupunguza janga la ajali barabarani nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo amebainisha kuwa kituo hicho kitajenga uwezo wa wataalam, kufanya tafiti, na kuweka mikakati itakayosaidia serikali na umma kwa ujumla kuimarisha usalama barabarani kupitia maamuzi yanayotokana na takwimu (data driven decision making).
Kwa upande wake Dkt. Prosper Mgaya, Mkuu wa chuo cha NIT, amesema kituo hicho kimeanzishwa kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kama mkakati wa serikali kukabiliana na janga la ajali barabarani.
“Tunapozungumzia kituo hiki, tunamaanisha kitakuwa kitovu cha tafiti, mafunzo na kampeni za uelewa kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kitahakikisha usalama wa barabara kuanzia hatua ya usanifu, ujenzi hadi matumizi yake,” alisema Prof. Mgaya.
Naye Mhandisi Kashinde Musa, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Mazingira Wizara ya Ujenzi na Mwenyekiti wa Bodi hiyo mpya, amesema chombo hicho kitapambana na changamoto kubwa ya ajali barabarani kupitia matumizi ya teknolojia.
“Tafiti zinaonesha zaidi ya asilimia 76 ya ajali nchini zinasababishwa na tabia za kibinadamu. Kama Bodi, tumejipanga kutumia teknolojia kupunguza changamoto hii, jambo ambalo pia ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mhandisi Musa.
Bodi hiyo mpya ni jumuishi, ikihusisha wajumbe kutoka taasisi mbalimbali zinazoshughulika na usalama barabarani zikiwemo TANROADS, LATRA, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya na Jeshi la Polisi ambapo wadau hao wamesisitiza dhamira ya Bodi kuhakikisha Tanzania inafuata miongozo ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo azma ya kupunguza ajali barabarani kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.