WATUMISHI WA TANROADS WASHIRIKI KUSAFISHA HOSPITAL YA RUFAA YA MKOA WA DODOMA
Dodoma
07 Agosti, 2024
Baadhi ya watumishi wa Wakala ya Barabara Tanzania(TANROADS), pamoja na kuwa na majukumu waliyopewa kisheria pia wanalo jukumu la kuhakikisha wanashiriki katika suala zima la utunzaji wa mazingira katika miundombinu yake pamoja na maeneo ya jamii.
Bw. Clement Ndagiwe, ambaye ni Fundi Sanifu Mwandamizi wa TANROADS akizungumza na vyombo vya habari tarehe 07 Agosti, 2024 mara baada ya kumaliza zoezi la kufanya usafi katika barabara zinazozunguka Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na viunga vyake, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa maonesho ya Wakulima ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini hapa.
"Tuna majukumu ya kusanifu, kujenga, kutunza na kukarabati miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na madaraja, ila tunapaswa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo hii ya kufanya usafi wa mazingira, katika miundombinu na katika maeneo yanayozizunguka jamii," amesema Bw. Ndagiwe.
Bw. Ndagiwe ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuwa na tabia ya kutunza mazingira , ili kuondokana na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza kutokana na kutupa takataka maeneo mbalimbali.
Amesema TANROADS wameamua kuchagua kufanya usafi katika eneo la hospitali kwa kuwa mahali hapo kuna wagonjwa wanaopata huduma za kitabibu, hivyo ni sehemu ya kijamii inayopaswa kuwa safi muda wote, ili kuleta faraja kwa watumiaji na watoa huduma kwenye hospitali hiyo.
"Ufanyaji usafi huu ni muendelezo wa kazi mbalimbali tulizofanya tangu tuwasili hapa Dodoma tukishiriki kwenye maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane, tumekuwa tukitoa elimu kwa umma kuhusu mambo mbalimbali tunayoyafanya," amesema Bw. Ndagiwe.
Naye Afisa Habari wa Hospital hiyo, Bi. Tumaini Mbwilo ameishukuru TANROADS kwa kuungana nao katika kufanya usafi wa mazingira ya hospital hiyo.
Kwa upande wake mkazi wa Ihumwa, amesema taasisi nyingine ziige mfano wa TANROADS katika kujumuika na jamii katika utunzaji wa mazingira.